Kanda ya KusiniKilimoMtwara

MUHOGO: zao tegemezi la wanyonge kanda ya kusini, lisilo na soko la uhakika

Muhogo ni zao la chakula ambalo hulimwa hapa nchini. Wengi wa wakulima wanaojihusisha na kilimo hicho ni watu wa kipato cha chini licha ya kutumiwa na watu wa madaraja yote kama chakula.
 
Zao hili hulimwa maeneo mbalimbali hapa nchini, ambapo  asilimia 75 ulimwa kwa ajili ya matumizi ya chakula na asilimia 25  ni kwa ajili ya  matumizi mengine. Muhogo unaweza kuutafuna ukiwa mbichi, kupika majani yake kama mboga, kuchemsha, kukaanga na hata kuusindika kwa ajili ya kupata unga.
 
Hata hivyo, wakulima wengi wanapenda kuchanganya zao hilo na mazao ya jamii ya kunde na mahindi ambayo ni tegemeo la chakula ili kujiongezea chakula ama kipato ambapo kwa mikoa ya kusini zao hilo baadhi ya watu hulifanya kama akiba ya dharura pale njaa inapotokea huku wengi wao wakidai halina soko la uhakika ndio sababu zinazopelekea kulimwa kwa kiasi kidogo.
 
Kwa mkoa wa Mtwara zaidi ya asilimika 80 ya wakulima wanaojishughulisha na kilimo kila mmoja lazima anakuwa na kiasi cha miti kadhaa ya mihogo kwaajili ya chakula cha nyumbani.
 
Kutokana na changamoto hizo shirika lisilokuwa la kiserikali la Mennonite Economic Development Associate (MEDA) linaloshughulikia kuondoa umaskini  kwa kutumia njia za kibiashara liliamua kutekeleza mradi wa majaribio wa kurasimisha mfumo wa upatikanaji wa mbegu bora za muhogo kwa kutumia njia za kibiashara ili kuwainua wakulima.
 
Licha ya jitihada ya Shirika hilo kuwawezesha wakulima hapa nchini kuzalisha mbegu za kisasa na kuzisambaza kwa wakulima wadogo wadogo vijijini, bado kasi ya wakulima kuitikia  kulima zao hilo ni ndogo ikilinganishwa na kilimo cha mazao mengine ya chakula na biashara.
 
Hali hiyo inatokana na mamlaka mbalimbali za serikali zikiwemo halmashauri za miji na wilaya na wizara ya kilimo uwangiliaji na ushirika  kutofanya jitihada za kuwatafutia soko wakulima.
 
Mkulima mzalishaji wa mbegu za muhogo aina ya kiroba wa kijiji cha Ndomoni, wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi Raymond Erasto ambaye amewezeshwa na MEDA anasema kuwa kwa sasa wakulima wachache wanaojishughulisha na kilimo cha muhogo wanalima kwa ajili ya matumizi ya chakula pekee hali ambayo inawafanya wakulima kutojitokeza kwa wingi kujishughulisha na kilimo hicho kwani hulima vijishamba vidogo ambavyo haviwezi kuwapatia tija.
 
Mzalishaji  huyo wa mbegu mwenye hekari tano ambapo hekari moja ina uwezo wa kupandwa miti 4,000 amekiri kwa muda wa miaka mitatu aliyojishughulisha na uzalishaji wa mbegu za muhogo licha ya kufanikiwa kupata kiasi kikubwa  cha fedha kwa kuuza mbegu ya muhoga kasi ya wakulima kununua mbegu ni ndogo hasa kwa wakulima wadogo wadogo ambao wanatabia ya kuomba mbegu na sio kununua.
 
“Changamoto kubwa ni kwa wale wateja ambao ni wanajamii, awali walitarajia kupata miti ya muhogo bila malipo, lakini angalau kwa sasa wamepata uelewa kuwa miti inauzwa Sh 200 ingawa bado kasi ni ndogo kwani zamani walikuwa na tabia ya kuombana mbegu,”anasema Raymond
 
Naye mzalishaji wa mbegu za muhogo wa kijiji  cha Lengo wilayani Newala mkoani Mtwara, Hamisi Kasembe anasema kwa muda wa miaka mitatu aliyokuwa mzalishaji wa mbegu za muhogo amekabiliwa na  changamoto ya soko la zao hilo licha ya kufanya jitihada mbalimbali kushawishi wakulima kutumia mbegu bora zenye ukidhani wa magonjwa.
 
Anasema mbegu ya muhogo kwa kipande kimoja cha mti anauza kati ya Sh 200 hadi Sh 300 lakini bado wakulima wengi wanaojishughulisha na zao hilo kwaajili ya chakula wana utamaduni wa kuomba mbegu na sio kununua.
 
“Nilipatiwa mafunzo na Meda pia nikakutana na wataalamu wa mbegu (TOSCI) na walinieleza mbegu bora na njia bora za kutumia, lakini licha ya kulima kilimo bora bado hatuna wateja wa kuwauzia mbegu licha ya kuwa nimekuwa nikiwashawishi lakini bado mwitikio ni mdogo kwasababu mtu anataka mbegu ya bure,” anasema Kasembe
 
Anasema kuwa licha ya kikundi chao hapo kijijini kuwa na mashine ya kusindika muhogo, bado soko la unga huo ni dogo hali inayofanya kutojishughulisha na usindikaji, badala yake kutegemea wanunuzi wachache wanaojishughulisha na biashara ya ukaangaji wa vitafunwa.
 
Geophrey Chilumba mkulima kutoka kata ya Chikukwe wilaya ya Masasi anasema zao la muhogo linaweza kubadili maisha ya wakulima endapo watafuata kanuni bora za kilimo kutoka kwa wataalamu na kuiomba serikali kuwa karibu na wazalishaji wa mbegu bora ili kuwa na uahakika wa soko.
 
“Naiomba serikali iweze kutujali wazalishaji wa mbegu mfano pale halmashauri inapohitaji mbegu kuzitawanya ituone sisi hii itatupa moyo,kama hivi sasa nazalisha mbegu zenye ukidhani na magonjwa lakini hakuna wateja,”anasema Chilumba
 
Naye Asha Namungulile ni mkulima kutoka kijiji cha Lengo kata ya Mchemo tarafa ya Kitangali wilaya ya Newala anasema miaka ya nyuma walikuwa wakijihusisha na kilimo cha kienyeji pasipo mafanikio lakini kwa sasa wamepata mbegu bora lakini wanakabiliwa na changamoto ya masoko.
 
“Zamani nilikuwa nafanya kilimo kwa kutumia mbegu za kienyeji ili nipate muhogo kwaajili ya chakula,lakini kwa sasa natumia mbegu bora baada yakununua mbegu bora ya kiroba kwa mkulima aliyenufaika na Meda ndipo na mimi nilipohamasika kuwa mzalishaji lakini kinachoumiza watu walishajijengea dhana ya kuombana mbegu,”anasema Namungulile
 
Kwa mujibu wa mkuu wa idara ya utafiti wa mazao ya jamii ya mizizi wa kituo cha utafiti cha Naliendele, Dr. Geofrey Mkamilo anasema kuwa Tanzania inazalisha tani milioni tano kila mwaka ambapo kati ya hizo kanda ya ziwa yenye mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Kagera, Simiyu, Mara na Geita ndio inayoongoza kwa kuzalisha asilimia 37 ya zao hilo.
 
Ukanda unaofuata kwa uzalishaji wa muhogo ni kanda ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Mtwara, Lindi na wilaya ya Tunduru ambayo uzalisha asilimia 25 ya mihogo yote hapa nchini.
 
Mtafiti huyo alibainisha kuwa kanda ya mashariki yenye mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga na Morogoro inazalisha asilimia 12 ikifuatiwa na kanda ya nyanda za juu kusini yenye mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi na Ruvuma ambayo uzalisha asilimia 10, kanda ya magharibi yenye mikoa ya Tabora na Kigoma inazalisha asilimia 6.
 
Kanda za kati zenye mikoa ya Dodoma na Singida na kanda ya Zanzibar inayojumuisha mikoa iliyopo visiwa vya Unguja na Pemba unazalisha asilimia 3 na ukanda wa mwisho ni kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara ambayo uzalisha asilimia moja ya muhogo wote unaozalishwa hapa nchini.
 
Dk Mkamilo anasema ukitaka kilimo bora ni lazima uanze kwa kuainisha mbegu bora zenye ukinzani wa magonjwa na zinazozaa sana kwa kuwatafuta wataalamu wa kilimo.
 
“Ukitaka kilimo bora lazima uanze na kilimo bora, lazima kuainisha mbegu bora zenye ukinzani wa magonjwa na zinazozaa sana, lakini changamoto iliyopo kwa baadhi ya wakulima ukiwaambia wanunue mbegu hawataki, kwasababu walishazoea kupeana mbegu jambo ambalo linasababisha hata mihogo kushambuliwa na magonjwa ya batobato na michirizi ya kahawia kwasababu mbegu wanayotumia haijathibitishwa na mtaalamu,”alisema Dk Mkamilo
 
Anasema yapo mafanikio ya kusambaza mbegu kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikwemo Meda ambapo anasema zaidi ya pingili milioni nne zimesambazwa kwa wakulima na kusema kwa kutumia maabara wameweza kuainisha virusi wanavyoweza kupambana navyo, ili kushauri wakulima na wadau kujua aina ya mbegu zinazoendana na mazingira yao na kubaini ni virusi aina gani.
 
“Zao la muhogo ni zao linalolimwa maeneo mengi, kwa kutumia maabara tumeweza kuanisha aina ya virusi tunavyoweza kupambana navyo ili kushauri wakulima na wadau wengineo kujua kujua aina ya mbegu zinazoendana na mazingira na kubaini ni virusi aina gani,” anasema Dk Mkamilo
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, Mhandisi Jackson Masaka anasema halmashauri hiyo mwaka huu wa fedha wametumia kiasi cha Shilingi 31 milioni kwa ajili ya kununulia mbegu za muhogo na ufuta na kuzisambaza kwenye vikundi vidogo vidogo vya wakulima na kwa bajeti ya mwakani halmashauri imetenga kutoka kwenye vyanzo vyake vya mapato shilingi 50 milioni ambazo zitatumika kwa ajili ya ununuzi wa miti ya muhogo na kusambaza kwa wakulima lengo ni kuongeza uzalishaji wa muhogo.
 
Mkuu wa idara ya ya kilimo, ushirika na umwagiliaji wa halmashauri ya Nachingwea, Raphael Ajetu alikiri kuwemo kwa tatizo la soko la muhogo na katika kukabiliana na hilo idara yake imeendelea kuhamasisha wakulima kulima zao la muhogo ambapo kila kata katika halmashauri hiyo inatakiwa na kuwa hekari kumi na kila mkulima lazima alime hekari moja ya muhogo kwani kuna kiwanda kinatarajiwa kujengwa mkoani Lindi kwa ajili ya kutengeneza wanga hivyo itasidia kutatua tatizo la soko.
 
“Licha ya halmashauri  kuviwezesha vikundi kwa kuvipatia viwanda vidogo vya kusindika muhogo bado tunatarajia  hivi karibuni  kitaanzishwa kiwanda cha wachina katika kijiji cha Mtama ambacho kitatua  kabisa kero ya soko la zao hili na halmashauri yetu imepitisha sheria kila kaya lazima iwe na hekari moja ya muhogo,”anasema Ajetu.
 
Naye meneja mradi wa Meda, Stephen Magige anasema mradi huo ulianza utekelezaji wake mwaka 2012 katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Dodoma. Baada ya kuonyesha mfumo wa kibiashara unafanya vizuri katika mikoa hiyo, Mfadhili wa mradi Bill and Belinda Gates foundation aliruhusu majaribio yafanyike katika kanda ya ziwa na pwani kuanzia mwaka 2012 ambapo mpaka sasa mradi unafanya kazi na wakulima wajasiliamali 156 katika ngazi mbali mbali za mfumo rasmi wa Mbegu.
 
Anasema wakulima wamekuwa wakipata mbegu za muhogo kutoka kwa wakulima wengine au wanagawiwa bure kutoka katika miradi ya serikali na taasisi ambapo njia zote hizi zinasababisha kueneza zaidi kwa  magonjwa ya batobato na michirizi ya kahawia na si endelevu.
 
Anasema Batobato na Michirizi ya kahawia ni magonjwa yanayoweza kupunguza uzalishaji kwa asilimia 80-100 hivyo mradi wao unajaribu njia ya kibiashara itakayoonyesha ni jinsi gani mkulima ataweza kupata mbegu bora za muhogo kwa njia endelevu.
 
“Mradi unawatumia wakulima wajasiliamali kuzalisha Mbegu bora na kuwauzia wakulima wengine tukiamini kuwa mjasiliamali ataendelea kuzalisha kwa kupata faida na mkulima ataendelea kununua kwa faida atakazozipata kutoka kwenye Mbegu bora. Lengo la mradi ni kuwaonyesha wadau,watunga sera na watu wote jinsi gani na vipi mfumo wa kibiashara unavyoweza kuhakikisha mbegu bora za muhogo zinawafikia wakulima kwa bei wanayoweza kuimudu na kwa njia endelevu,”anasema Magige na kuongeza
 
“Wazalishaji hawa wa Mbegu bora za Muhogo wamepewa mafunzo ya uzalishaji bora wa Mbegu,wamesajiliwa kama wazalishaji na wizara ya kilimo na mashamba yao yanakaguliwa na taasisi ya uthibiti wa Mbegu TOSCI kabla hawajaruhusiwa kuuza Mbegu zao kwa wakulima na ili kuwawezesha kushiriki katika majaribio haya wakulima wazalishaji wa mbegu wanasaidiwa gharama za uandaaji ,usimamizi na pembejeo na mradi,”anasema Magige

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Close