ElimuKanda ya KusiniMtwara

Usiri na kutengwa viongozi wa kijiji kwachangia wanafunzi kufeli Mtwara

Imebainika kuwa wanafunzi 22 waliofeli mtihani wa kipimo wa kidato cha pili 2016 katika shule ya sekondari Mtiniko halmashauri ya Mji Nanyamba wilaya Mtwara mkoani hapa walikuwa hawajui kusoma na kuandika.

Mtiniko ni moja kati ya shule tisa za mkoa wa Mtwara zilizofanya vibaya katika mitihani ya kidato cha pili 2016.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaii kuwa wanafunzi hao ni kati ya 89 waliofeli mtihani huo

Shule hiyo ambayo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007 haijawahi kuwa na mwalimu Hisababti na Fizikia ipo zaidi ya kilomita 45 kusini mashariki mwa Mji wa Mtwara ilikuwa na watahiniwa 144, kati ya wanafunzi 150 waliosajiliwa ambapo 55 pekee ndiyo walioweza kuruka kihunzi hicho (kufaulu).

“Unaweza kujiuliza inawezekanaje mwanafunzi asiyejua kusoma na kuandika Kiswahili aliwezaje kufaulu mtihani wa darasa la saba…tuliwapokea wanafunzi 150 baada ya upembuzi tukagundua kuwa 22 kati yao walikuwa mambumbumbu lakini tuliendelea kuwafundisha” anasema Lwitiko Mwakabende makamu mkuu wa shule hiyo.

“Kama alishindwa kujua kusoma na kuandika kiswahili kwa miaka Saba tunataraji ndani ya miaka miwili ajue kusoma na kuandika kiingereza, sidhani kama kuna muujiza wa kufanikisha hilo” anasisitiza Mwakabende

“Tumekuwa na wanafunzi watoro wa kudumu kabisa zaidi ya 40,lakini ukija kuangalia wale wanaokuja kwa wiki mara mbili au moja ni kama wanafunzi 30 anakuja wiki hii wiki ijayo hayupo, kwahiyo unakuta tulikuwa na watoro ambao hawaingii darasani zaidi ya 70 kwa kidato pili tu,”anabainisha mwalimu huyo Mwakabende na kuongeza;

“Wanafunzi Sita walishindwa kufanya mitihani kutokana na utoro, watatu kati yao walipata mimba…kutokana na utoro wanafunzi hawa walipoteza ari ya kujisomea, katika mzingira hayo ni vigumu kufanya vizuri katika mitihani yao…

Mbali na utoro kuna wanafunzi  ambao utayari wao ni mdogo kuendelea na shule lakini mzazi nyumbani ni mkali ili mtoto azingatie shule, lakini mtoto ili kumkomesha mzazi walichokifanya ni kuunda makundi ya kufanya vibaya mtihani ili wasiendelee na shule na kweli kundi hilo lote limeanguka”

Anaeleza kuwa walimu wameyabaini hayo baada ya mtihani kumalizika na wao kupata taarifa kutoka kwa wanafunzi wengine juu ya uwapo wa kundi lililojipanga kufanya vibaya ili wasiendelee na shule.

“Shule hii inahudumia wanafunzi wa kata mbili ya Mtiniko na Mtimbwilimbi, wapo wanafunzi wengine wanatoka mbali sana, kwahiyo utakuta mwanafunzi hafiki shule kwa madai baiskeli iliharibika, lakini pia umbali huo unagharimu wanafunzi kwa sababu hata akitoka hapa saa nane hadi kufika nyumbani ni jioni unakuta ameshinda na njaa,” makamu mkuu huyo wa shule anafafanua changamoto zinazoikabili shule hiyo

“Tangu shule ianze mwaka 2007 haijawahi kuwa na mwalimu wa hesabati na fizikia, hii ndiyo kusema kabla ya mtihani wanafunzi tayari wanakuwa wamefeli masomo hayo mawili…kimsingi changamoto ambazo zipo chini ya uwezo wetu tutakabiliana nazo na zile zilizopo nje ya uwezo wetu tunaomba wahusika watusaidie,” anatoa rai Mwakabende

Mwenyekiti wa kijiji cha Mbambakofi ilipo shule hiyo,Hamis Dadi anasema sababu za kufanya vibaya zinatokana na uhaba wa walimu waliopo katika shule za msingi kwasababu elimu ya msingi ndio inayoanza kumjenga mtoto pamoja na utayari wa mwalimu mwenyewe kumfundisha mtoto.

“Matokeo mabaya yanachangiwa na kutowepo kwa walimu wa kutosha shule za msingi,inawezekana hawapati elimu ya kutosha ya awali kwasababu ndio inayomjenga,lakini hata wale walimu wachache waliopo wawe na utayari, serikali iwatie motisha wakubaliane na uchache wao wawasaidie watoto wetu,”anasema Dadi

Rehema Ismailni mmoja wa wazazi mwenye mtoto aliyepo sekondari lakini anasema amekuwa hafuatilii maendeleo ya mwanaye kutokana na kulelewa na baba yake baada ya kutengana.

“Matokeo mabaya yanasabishwa na watoto kulelewa na mzazi mmoja,mfano mimi mwanangu simfuatilii kwasababu anakaa na baba yake sisi tuliachana,”anasema Ismail

Naye mzazi Mohamed Hamad anasema kama mzazi akielimishwa ni rahisi kufuatilia maendeleo ya mtoto.

“Wazazi mkituelimisha sasa tunaelimika sio kama miaka ya 80,sababu za utoro ni wazazi hawajawa tayari kwasababu wanafunzi wenyewe ukiwaambia wasome wanasema kichwani hamna kitu na hata wale wanaokwenda hatujui kama wanafika shuleni,”anasema Hamad

Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Nanyamba ambaye pia ni afisa elimu sekondari ,Bumi Kasege anakiri wamekuwa wakikumbana na chagamoto ya wanafunzi wasiojua kusoma, kuhesabu na kuandika huku baadhi wakisoma neno  moja moja huku wengine wakishindwa kabisa.

Anasema sababu hiyo inachangiwa na aina ya mtihani wenyewe kutokana na kuwa  na maswali ya kuchagua na kushade (kuweka kivuli) pekee hivyo mwanafunzi mwingine anaweza kuibia kwa wenzake au kubahatisha na kufaulu.

“Inatokana na aina ya mtihani mtoto anaweza akawa amekaa karibu na wenye uwezo sababu unakuta maswali yote ni ya kuchagua na kuweka kivuli kwahiyo anaweza akaangalia kwa mwenzake na mwingine ikawa ni bahati yake anabahatisha akapatia,”anasema Kasege

Aidha alikiri uwepo wa uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi,hisabati na biashara.
Anasema katika halmashauri hiyo inahitaji walimu wa sayansi na hisabati wapatao 86 lakini waliop ni 31na walimu wa masomo ya biashara wanaohitajika ni 4.

Viongozi wa vijiji kutengwa chanzo cha matokeo mabaya
Kitendo cha baadhi ya viongozi wa ngazi za vijiji na mitaa kutoshirikishwa katika masuala mbalimbali ya elimu kimedaiwa ni mojawapo ya sababu zinazochangia kuporomoka kwa elimu.

Viongozi hao wamedai mara nyingi wamekuwa wakitafutwa hasa pale kunapokuwa na tukio hasi katika jamii ndipo uwapo wao unapotambuliwa na si kushirikishwa kabla ya kutokea kwa jambo husika.

Viongozi hao wanalalamika
Ally Ndumbe ni mtendaji wa kijiji cha Mbambakofi anasema anashangazwa na viongozi wa ngazi za juu kuwadharau na kutowashirikisha katika kusimamia elimu ili hali wao ndiye wenye watu wanaowaaongoza

Anasema walimu na viongozi wengine wamekuwa wakikimbilia kuripoti matatizo ya shule na wanafunzi katika ngazi za juu bila kuwashirikisha ili hali ufumbuzi wake ungeweza kupatikana ndani ya kijiji.

“Mara nyingi nimekuwa nikisikia kwenye vyombo vya habari kuwa matokeo ni mbaya na sababu ikidaiwa ni utoro kwa wanafunzi, lakini watunga sera wametusahau sisi viongozi wa vijiji na mitaa katika kupanga mikakati ya kuboresha elimu, kukiwa na shida ndipo utaona mtendaji wa kijiji au mwenyekiti unatafutwa,”anasema Lidumbe na kuongeza

“Kwa mfano tatizo la utoro tungeweza kulimaliza kwa kuitisha mkutano wa kijiji na kuongea na wananchi wote kwa ujumla na kukubaliana mikakati ya pamoja na kudhibiti hali hiyo…ajabu baada ya matokeo mabaya ndo nasikia kupitia redio sababu ni utoro”

Naye Hamis Dadi mwenyekiti wa kijiji hicho anasema imefikia kipindi uongozi wa baadhi ya shule katika maeneo yao wamekuwa wakiwatafuta hasa panapotokeo ugomvi wazazi na walimu.

“Kofia ya mwenyekiti wa kijiji katika elimu haitambuliki lakini ukitokea ugomvi wa mwalimu na mzazi ndipo mwenyekiti natafutwa, hakuna uongozi mwema kati ya viongozi wa kijiji na shule, hata watunga sera hawachanganyi walimu na viongozi wa vijiji lakini cha kushangaza wanapotaka kuongea na jamii ndipo utasikia mwenyekiti ukiambiwa itisha mkutano na unaishia kuwa mtu wa kufungua mikutano na kufunga basi,”anasema Dadi na kuongeza

“Mfano baadhi ya shule zetu zina mikorosho wanapovua zile korosho hutoona wakikushirikisha chochote lakini ikitokea labda zikaibiwa umuhimu wako ndio unaonekana, na wakati mwingine wenye mamlaka wanapotoa semina wanawachukua tu wajumbe wa bodi za shule lakini wale wanakuwa hawana nguvu ya kuwaita wananchi na kuwashirikisha walichozungumza katika semina.

Uwazi
Amina Ally ni mkazi kijiji cha Mbambakofi ambako shule ya sekondari Mtiniko ambayo ni miongoni mwa shule zilizofanya vibaya ipo anasema hakuwahi kupokea taarifa zozote zinazohusiana na matokeo zaidi ya kusikia kupitia vyombo vya habari.
Anasema  wao kama wanakijiji wanapoitwa katika vikutano hujadiliana mambo mbalimbali lakini elimu haipewi kipaumbele inavyotakiwa.

“Kuna nini kimejificha kwanini hatushirikishwi, mfano matokeo mabaya yanayozungumziwa leo niliyasikia kupitia redio lakini uongozi wa shule ulikuwa na nafasi ya kuongea na serikali ya kijiji ukaitwa mkutano wa pamoja tukajadiliana kwa pamoja , zaidi tutaambiwa tujitolee labda kujenga madarasa au nyumba ya mwalimu,”anasema Ally

Makamu mkuu wa shule ya sekondari Mtiniko, Mwalimu LwitikoMwakabende ameeleza wamekuwa wakishirikiana vyema na jamii katika suala nzima la elimu hali inayowapeleka hata wanakijiji kushiriki katika ujenzi wa nyumba za walimu.

“Mahusiano yetu na jamii yako tu vizuri kama hivi katika ujenzi wa nyumba za walimu walijitolea nguvu kazi mpaka tukafanikiwa kuijenga nyumba pamoja na kisima kwasababu mazingira ya shule kuna tatizo la maji,’anaeleza Mwakabende
Wazazi kuwapa walimu jukumu la kulea watoto wao

Makamu mkuu wa shule anasema  wao kama shule wamekuwa wakijitahidi kutekeleza wajibu wao kama inavyotakiwa lakini kuna wakati baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwapa walimu jukumu la kurudisha nidhamu kwa watoto wao hasa wanapowashindwa katika jamii.

“Mwalimu kama mwalimu pekee hawezi kumlea mwanafunzi lakini wakati mwingine wazazi wanakuja kututupia mizigoya watoto kutokana na kukataa shule kwahiyo anakuwa anaomba msaada lakini inafikia mahali mwalimu anashindwa kwasababu mwalimu yeye anamsimamia mwanafuzi akiwa shuleni,’anasema

Kutokana na hali hiyo mwenykeiti wa kijiji , Hamis Dadi anasema ni vyema walimu kujipanga katika masuala ya elimu na wao kama jamii wasimamie mienendo ya wanafunzi pindi wanapokuwa uraiani ili kuboresha elimu.

“Kama kila mmoja akitambua wajibu wake basi elimu itakuwa nzuri, walimu wajipange katika masuala ya elimu na sisi jamii tuelimishe watoto nini umuhimu wa elimu, naamini kama tukishirikiana na kila mmoja kutambua mchango wa mwenzake tutanyanyua elimu na hata na hata wenye madaraka wanapoanga mambo ya elimu wasituache sisi viongozi ambao ndio tuna nguvu kwa jamii,’anasema Dadi.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Close