Simanjirowajasiriamali kinamama

Wajane Simanjiro wahamasishwa kuwa wabunifu

Wajasiriamali wajane wa kikundi cha Upendo cha Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakimuonyesha Mkuu wa Wilaya hiyo, mhandisi Zephania Chaula (kushoto) namna wanavyotengeneza vitambaa vyao vya batiki.

Wajasiriamali wajane wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kutokata tamaa na kulalamikia ugumu wa maisha ila waongeze juhudi na kuwa wabunifu wa shughuli zao.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula, aliyasema hayo wakati akizungumza na wajasiriamali wajane wa kikundi cha Upendo cha mji mdogo wa Mirerani.

Mhandisi Chaula alisema wajane hao wakijishughulisha na kufanya kazi kwa bidii bila kukata tamaa, watafika mbali na kuwa na maendeleo mengi kuliko kubaki kulalamika na kujihisi wanyonge.

Alisema shughuli zao za ujasiriamali za kutengeneza mavazi ya batiki, majiko na kazi nyingine zinaweza kuwapa kipato kikubwa na kuendeleza kazi nyingine ambazo ni kubwa zaidi ya hizo.

Alisema kupitia fursa hiyo wanayoifanya kwa kupitia kikundi chao cha wajane wa Upendo na shughuli zao ujasiriamali huo wanazozifanya wakiziendeleza kwa bidii, juhudi na maarifa wataona manufaa yake.

“Msijisikie unyonge na kujiona ninyi ni watu wa nyuma kwa sababu ya kuwa wajane hapana hiyo ni changamoto igeuzeni kuwa fursa jamani mbona wagane huwa hawalalamiki,” alisema mhandisi Chaula.

Wajasiriamali wajane wa kikundi cha Upendo cha Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakimvisha Mkuu wa Wilaya hiyo, mhandisi Zephania Chaula (kushoto) baada ya kuwatembelea na kuona namna wanavyotengeneza vitambaa vyao vya batiki. Picha zote na Joseph Lyimo

Katibu wa kikundi cha wajane cha Upendo, Ania Rashid alisema kikundi chao kilianzishwa mwaka 13 Aprili 2015 kikiwa na wanachama 85, wanne walifariki, wengine walihama sasa wapo wanachama 62.

Alisema mtaji mkubwa wa ujasiriamali wanaoupata wanategemea ada wanazolipia sh1,000 kwa kila mwanachana na wanatunisha mfuko wao kupitia fedha hizo wanazoendeleshea shughuli zao.

“Ili kutunisha mfuko wetu kuna mfadhili wetu aitwaye Theresia wa Palila, ambaye ni mchimbaji wa madini ya Tanzanite aliyetupa udongo wa mgodini kisha tukapata fedha za kujiendesha,” alisema Rashid.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Close