kanda ya ziwa

Wawili mbaroni, katika doria ya polisi kwa wanaochoma nyumba za wanyonge.

Wakaazi wa kata ya Mahyondwe wilayani Muleba mkoani Kagera, wameishi kwa hofu katika kipindi cha kuanzia mwanzoni mwa mwezi jun mwaka huu, kutokana na makaazi yao kuchomwa moto na watu wasiojulikana, ilhali watu wawili wakipoteza maisha katika halmashauri ya Karagwe kwa kuungulia ndani ya nyumba.

Baada ya wanyonge kuibua malalamiko yao kwa kukosa utatuzi kwa kipindi cha mwezi mzima, Polisi Mkoani Kagera imewakamata washukiwa wa kwanza wa matukio ya uchomaji moto nyumba zinazofikia 15 mpaka sasa wilayani Muleba.

Kamanda wa polisi mkoani Kagera Augostin Ollomi, ameieleza sautiyamnyonge kuwa watu hao walikamatwa kufuatia tukio lingine la uchomaji nyumba ya mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Protaz Karuya, mwenye umri wa miaka 60, na mkaazi wa kijiji Bugasha kata Mayondwe katika halmashauri ya wilaya Muleba.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Badrul Daniel wa miaka 32, msubi na mkazi wa kitongoji Ibara, na Angela Karisti mwenye miaka 36,muhaya na mkazi wa kitongoji Bisole kata Muhutwe. Amesema kuwa kukamatwa kwa watu hao kumetokana na taarifa za mtu mwenye mahusiano na mtuhumiwa aliyebainika kujihusisha na tukio la kuchoma nyumba hiyo na kukimbilia kusikojulikana.

Wakati huo huo polisi mkoani Kagera inashughulikia taarifa za wanandoa wawili kuungulia kwenye chumba wakiwa wamelala.

Amewataja marehemu hao kuwa ni Rameck Masinde aliyekuwa na miaka 64, na Katarina Lameck mwenye miaka 33, wote wanyambo na wakazi wa Karagwe katika tukio lililotokea julai pili mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Close