AfyaKanda ya KaskaziniMaji

Wakorea wawezesha mradi wa maji safi kwa wakazi 700 wa Irmorijo kuzinduliwa

Mkurugenzi wa kampuni ya Smart Vision ya Korea, Seo Young Kim akimuangalia Andrew Chung mbunifu wa mtambo wa kusafisha maji akionyesha mtambo huo kwenye uzinduzi wake kwenye kitongoji cha Irmorijo Kijiji cha Emairote Wilayani Monduli Mkoani Arusha.

Zaidi ya kaya 700 za wananchi wanyonge wa Kitongoji cha Irmorijo Kijiji cha Emairete Wilayani Monduli Mkoani Arusha, waliokuwa wanatumia maji ya kwenye bwana wanatarajia kunufaika na mradi wa kusafisha maji na kuchuja maji kuwa safi uliozinduliwa Kijiji hapo. 

Awali, wananchi hao wanyonge walikuwa wanatumia kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kupika, kufua, kuoga na kunywa maji hayo ya bwawa ambayo pia yalikuwa yanatumiwa na mifugo ya eneo hilo. 

Mkurugenzi wa kampuni ya Smart Vision ya Korea, Seo Young Kim akizungumza jana kwenye uzinduzi wa mradi alisema lengo ni jamii ya wanyonge eneo hilo kunufaika na maji safi na salama yanayochujwa kupitia ubunifu wao. 

Kim alisema kwa kuanza kuwanufaisha wananchi wa eneo hilo, wanatarajia kugawa majiko rafiki ya mazingira 22 na mitambo ya kuchuja na kusafisha maji ya bwawa kuwa safi na salama 22 kwa kaya 22 zitakazowanufaisha zaidi ya watu 220. 

 Alisema Smart Vision kupitia uwekezaji wa Korea Trade-Investment Promotion Agency. (KOTRA) jamii ya eneo hilo itanufaika na na mradi huo wenye lengo la kuondokana na matumizi ya maji yasiyo safi wala salama ambayo yanasababisha magonjwa ya tumbo. 

"Jamii ya eneo hili kupitia mchungaji wa kanisa la Enyorata Daniel Vengei, walileta maombi kwetu kuwa wanatatizo la maji, hospitali na shule, ndipo tukaona tuanze kutatua hili suala la maji ndipo tukaleta mitambo hii ya kuchuja na kusafisha maji," alisema Kim. 

Mkazi  mnyonge wa Kitongoji cha Emairete Rose Lemomo alisema alisema awali walikuwa wanakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama lakini kupitia mradi huo wataondokana na maradhi ya tumbo yaliyokuwa yakiwakabili hasa watoto. 

Lemomo aliwashukuru wote waliohusika na kufanikisha mradi huo, kwani hivi sasa watakuwa wanachota maji bwawani na kuyachuja na kuyasafisha kupitia mitambo hiyo. 

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Irmorijo, Mirishi Songoyo alishukuru shirika la Smart Vision kwa kufanikisha mradi huo wa maendeleo ambao utainufaisha jamii ya eneo hilo walioteseka kwa muda mrefu juu ya suala la maji. 

"Tunawaomba wananchi watakaofikiwa na mradi huu kuhakikisha wanawasaidia na wale ambao bado wanasubiri kupatiwa majiko na mitambo ya kuchuja na kusafisha maji," alisema Songoyo.  

Mwalimu wa shule ya msingi Irmorijo, Stephen Laizer aliwataka wananchi wote waliofanikiwa kupatiwa mradi huo kuhakikisha wanautunza ili kunufaika nao kwa muda mrefu kwani wameteseka kwa miaka mingi kwenye tatizo la maji. 

"Wageni wanapokuja kwenu inawabidi kuwashukuru hata kama hawajaacha chochote ila hawa wametuletea teknolojia ya maji, wanaweza kutufanyia mengine mazuri," alisema Laizer. 

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Close